Wakati wengi wanafikiria kuhusu uwekezaji, mara nyingi huwaza kuhusu kupata "gawio" (dividends) kila mwaka. Lakini kuna njia nyingine kubwa na muhimu sana ya kupata faida, nayo inaitwa "Capital Gain" au kwa Kiswahili chepesi, "Ongezeko la Mtaji."

"Capital Gain" ni Nini Hasa?

Kwa lugha rahisi kabisa, Capital Gain ni faida unayopata pale unapouza mali (kama hisa, kiwanja, au nyumba) kwa bei ya juu kuliko ile uliyoitumia kuinunua.

Ni ile "faida ya juu" unayoweka mfukoni baada ya kuondoa pesa yako ya mwanzo (mtaji wako).

Jiunge na Jamii ya Wasomaji

Kuwa sehemu ya jamii yetu na upate makala mpya, maudhui maalum, na mengi zaidi!

Kuwa Msomaji

Kanuni yake ni:

Bei ya Kuuzia - Bei ya Kununulia = Capital Gain (Ongezeko la Mtaji)

Capital Gains Katika Masoko ya Hisa Kama DSE

Tuseme tuna muwekezaji "Bwana Juma"

1. Hatua ya Kwanza: Kununua (Uwekezaji wa Mwanzo)

  • Mwaka 2018, Bwana Juma alinunua hisa 10,000 za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wakati wa IPO.

  • Bei ya hisa moja ilikuwa: TSh 500

  • Jumla ya Mtaji alioweka (Gharama): 10,000 hisa * TSh 500 = TSh 5,000,000

2. Hatua ya Pili: Kushikilia (Uvumilivu)

  • Bwana Juma hakuziuza hisa zake. Aliamua kuzishikilia kwa miaka kadhaa. Katika kipindi hicho, kampuni ya DSE ilifanya vizuri na thamani ya hisa zake sokoni ikapanda.

3. Hatua ya Tatu: Thamani ya Sasa (Ongezeko la Thamani)

  • Leo, bei ya hisa moja ya DSE ni TSh 6,800.

  • Thamani ya hisa za Bwana Juma sasa ni: 10,000 hisa * TSh 6,800 = TSh 68,000,000

4. Hatua ya Nne: Kuhesabu Faida (Capital Gain)

  • Kama Bwana Juma akiamua kuuza hisa zake zote leo, atapata TSh 68,000,000.

  • Tukitumia kanuni yetu:

  • Bei ya Kuuzia (TSh 68,000,000) - Bei ya Kununulia (TSh 5,000,000) = TSh 63,000,000

Mambo Muhimu ya Kujua Kuhusu Capital Gain

Kuna mambo mawili muhimu ya kutofautisha:

1. Faida ya Kwenye Karatasi (Unrealized Gain)

Hadi pale Bwana Juma anapobonyeza button ya kuuza na kuuza hisa zake, ile TSh 63,000,000 ni "faida ya kwenye karatasi" (unrealized gain). Inamaanisha thamani ya mali yake imeongezeka, lakini bado hajapata pesa mkononi. Faida hii inaweza kupanda (kama hisa ikienda TSh 7,000) au kushuka (kama hisa ikishuka TSh 6,500) kabla hajauza.

2. Faida Halisi (Realized Gain)

Siku Bwana Juma anapouza rasmi hisa zake na pesa kuingia kwenye akaunti yake ya benki, hapo anakuwa amepata "faida halisi" (realized gain).

Capital Gain Ipo Kwenye Nini Kingine?

Mfumo huu wa "Ongezeko la Mtaji" haupo kwenye hisa pekee. Unatumika pia kwenye:

  • Viwanja na Nyumba (Real Estate): Unanunua kiwanja Mbezi kwa TSh 20M, unakishikilia miaka mitano, unakuja kukiuza kwa TSh 80M. "Capital Gain" yako ni TSh 60M.

  • Dhahabu na Madini: Unanunua gramu za dhahabu bei ikiwa chini, unauza bei ikipanda.

  • Hati Fungani (Bonds): Ingawa hizi zinajulikana zaidi kwa riba (coupon), zinaweza pia kuuzwa kwa faida kabla ya muda wake kuisha.

Mwisho: Usisahau Kodi

Ni muhimu kukumbuka kwamba katika nchi nyingi, ikiwemo Tanzania, hii "Capital Gain" (faida halisi baada ya kuuza) huwa inatozwa kodi. Inaitwa "Kodi ya Ongezeko la Mtaji" (Capital Gains Tax). Hivyo, siyo faida yote ya TSh 63,000,000 ndiyo itaenda mfukoni; kiasi fulani kitakwenda serikalini kama kodi.

Kwa kifupi, "Capital Gain" ndiyo lengo kuu la wawekezaji wengi wa muda mrefu—kununua mali yenye uwezekano wa kukua thamani na kuja kuivuna baadaye.